Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Al-Houthi alionya dhidi ya hatari ya baadhi ya tawala za Kiarabu kushirikiana na mpango wa Marekani na Israel wa kuondoa silaha za mataifa ya eneo, akisisitiza kuwa tatizo si silaha za wapiganaji huru wa umma, bali ni silaha na mipango ya adui wa Kizayuni inayolenga kuondoa nguvu za kujihami za mapambano.
Katika hotuba iliyotangazwa kupitia vyombo rasmi vya habari vya Sana’a, al-Houthi alisema kuwa silaha za mapambano kwa miongo kadhaa zimekuwa kizuizi kikubwa dhidi ya utekelezaji wa mradi wa “Israel Kubwa”, na kwamba kukubali kuondoa silaha ni sawa na kujisalimisha na kuwa watumwa wa mpango wa wazi wa Kizayuni.
Alimkosoa vikali ukimya wa viongozi wa Kiarabu mbele ya matamshi ya dharau ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akieleza kuwa wavamizi hutekeleza miradi yao kulingana na utamaduni na imani zao, na kwamba uhalifu wa kila siku nchini Palestina na Lebanon kwa ushirikiano wa Marekani ni ushahidi wa wazi wa asili ya adui huyu.
Vilevile, aliwataka wanazuoni na wasomi kulinda na kutetea ukweli wa Qur’ani kuhusu hatari ya Uzayuni.
Katibu Mkuu wa Ansarullah alilituhumu serikali ya Lebanon kwa usaliti wa wazi, akisema kuwa kukubali mpango wa Marekani uliojaa masharti ya Kizayuni kunahatarisha usalama na mshikamano wa kitaifa wa nchi hiyo. Alionya kuwa mpango huo unakusudia kuibua fitna za ndani na kuibadilisha serikali ya Lebanon kuwa polisi wa Israel.
Al-Houthi pia alilaani uzembe wa nchi za Kiarabu mbele ya uvamizi wa Israel, akibainisha kuwa baadhi ya nchi za Ulaya zimeisimamisha biashara na Tel Aviv, huku tawala za Kiarabu zilizokubali maelewano zikiwa hazijachukua hatua yoyote.
Aidha, alitangaza kufanyika kwa operesheni ya kijeshi dhidi ya meli inayohusiana na kampuni mshirika wa Israel katika Bahari Nyekundu, akisema kuwa mashambulizi ya kuunga mkono Gaza ndani ya ardhi za Palestina zilizokaliwa yataendelea.
Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Yemen, Yahya Saree, operesheni hiyo ilifanywa kwa kombora la “Palestine 2” na kulenga Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion, jambo lililosababisha maelfu ya walowezi kukimbilia kwenye hifadhi na kusimamishwa kwa safari za ndege. Vyombo vya habari vya Israel, ikiwemo Yedioth Ahronoth, viliarifu kuthibitisha shambulizi hilo.
Wakati huohuo, jeshi la majini la Yemen limetangaza kanuni mpya za kuhakikisha usalama wa meli ambazo hazishirikiani na Israel katika Bahari Nyekundu na Bab al-Mandeb, likieleza kuwa meli zisizo katika orodha ya vikwazo zinaweza kupita kwa uhuru mradi tu zifuate sheria za baharini za Yemen.
Your Comment